Corona ilivyomuathiri beki Azam FC

Category: 
Team: 
Azam FC

BEKI wa kulia wa Azam FC, Nickolas Wadada, ameweka wazi kuwa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) limemuathiri kiuchumi baada ya kulazimika kuwasamehe kodi wapangaji wake.

Wadada kwa sasa yupo nchini kwao Uganda, akichukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Corona unaoendelea kuitesa dunia hivi sasa.

Mara baada ya ugonjwa huo kushika kasi miezi miwili iliyopita, serikali ya Uganda kupitia kwa Rais wake, Yoweri Museveni, uliwapa maelekezo wamiliki wote wa nyumba za kupanga kutowatoza kodi wapangaji wao katika kipindi hiki cha Corona.

“Nina nyumba ya kupangisha ambayo hunipatia pesa lakini kwa kuwa sasa tumekumbwa na janga la COVID-19 nimewasamehe kodi wapangaji wangu kama ambavyo Rais wetu Museveni alivyotuambia,” alisema Wadada wakati akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz

Mbali na janga la Corona kuathiri uchumi duniani, pia imepelekea kusimamishwa kwa shughuli za michezo duniani, ikiwemo Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ambayo ni takribani miezi miwili sasa tokea isimamishwe.

Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Magufuli, alitoa kauli yenye matumaini ya kurejea kwa ligi hiyo baada ya kusema kuwa anafikiria kuruhusu ligi hiyo iendelee tena siku za mbeleni kwa sababu hajasikia ugonjwa huo kuathiri mwanamichezo yoyote nchini.

Back to Top